Huduma mashuleni ni huduma inayojishughulisha na uinjilishaji wa neno la kristo katika shule mbalimbali za sekondari na vyuo. Huduma hii iko chini ya karesmatiki katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam, hivyo imepewa dhamana ya kuhudumia wanafunzi wanaohitaji huduma za kiroho.
Huduma hii ya uinjilishaji mashuleni, hufanya huduma zake katika siku tofauti katika juma. Wanafunzi hupata nafasi ya kukutana siku ya Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.
Siku ya Jumatatu, wanafunzi au vijana walioamua kujitoa kwa ajili ya Kristo, hukutana kwa ajili ya kujifunza neno la Mungu, lakini siku hii imewekwa maalum kwa ajili ya malezi ya kiroho, hivyo wanafunzi hupata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali ya kiroho.
Siku ya Jumatano, vijana pia hukutana kwa ajili ya kusifu, kuabudu na kusikiliza neno la Mungu. Wanafunzi kutoka shule mbalimbali hufika siku hii kwa ajili ya sala na maombi.
Siku ya Ijumaa pia kunakuwa na kusanyiko la wanafunzi pale Don Bosco Upanga, hukutana kwa ajili ya kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na maigizo na uimbaji. Baada ya darasa hilo kuisha hukutana pamoja kwa ajili ya fellowship ya pamoja.
Siku ya Jumamosi ni siku ambayo wanafunzi wengi hupata nafasi ya kufika kwenye fellowship kwa sababu siku hii wengi huwa hawaendi shuleni. Hivyo hufika Msimbazi Centre kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka saa 8:00 mchana kwa ajili ya maombi pamoja na ushauri. Pia hupata nafasi ya kuonyesha vipawa vyao vya kuimba na kuigiza katika siku hii. Kwa siku ya Jumatatu na Jumatano, hukutana hapohapo msimbazi centre kuanzia saa 10:00 jioni mpaka saa 12:00 jioni.
Pia kila Jumapili ya mwisho wa mwezi huduma mashuleni huandaa siku ya kuishi pamoja ambapo wanafunzi kwa kushirikiana na uongozi wa huduma huiandaa siku hii. Siku hii wanafunzi hufika pamoja na wazazi au walezi kwa ajili ya kusali pamoja, kula pamoja na vijana hao huonyesha mambo mbalimbali wanayojifunza katika huduma ikiwemo michezo inayotumika katika kuinjilisha kama maigizo na nyimbo. Siku hii huitwa siku ya familia, wilaya zote tatu yaani Ilala, Temeke na Kinondoni hukutana pamoja kama familia moja. Pia mbali na kukutana pamoja, familia, yani kila wilaya, hupata nafasi ya kukutana kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ya kimasomo pamoja na kufahamiana zaidi.