Monday, October 1, 2012

PATA UFAHAMU ZAIDI KUPITIA NENO:

Maandalizi ya Moyo: Heart Preparation.
BY: RAYMOND ANTONY.

                “Hakuna madhihirisho pasipokuwa na maandalizi”
          “There is no manifestation without preparation…”
Mit 16:1
“Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.”


         Siku zote neno la mwenye moyo safi hupokelewa na Mungu. Hivyo moyo ni eneo muhimu linalopaswa kuandaliwa kabla ya kwenda kukutana na Mungu. Kwa lugha rahisi, moyo ni madhabahu itumikayo kuweka sadaka iliyo safi mbele za Bwana.

Maandalizi makubwa ya moyo, huleta madhihirisho makubwa.


taz. (1fal 18:21-29) “…Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeneza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. ….. wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeneza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri…. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.”

         Mdahalo huu, baina ya Eliya na manabii wa Baali, ulikuwa unahitaji kuonyesha uwezo wa mungu ambaye aliaminika ana nguvu kutoka kila upande, yaani Mungu wa Eliya au mungu Baali. Hivyo maandalizi yalihitajika ili kufanikisha adhma zao.

Kwa upande wa manabii wa Baali walioanza walifanya maandalizi yao “….wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa wakamtengeneza,…” Maandalizi yao yaliangalia zaidi ile sadaka iliyotolewa (ng’ombe) kuliko madhabahu.


         Kwa upande wa Eliya nabii wa Mungu aliye hai alijiandaa namna hii; taz (1waf 18:30-35) “…Kisha Eliya akawaambia watu wote, nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo,…Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni,akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni…”


         Maandalizi makubwa ya moyo (madhabahu) huleta madhihirisho makubwa na ushindi. Eliya aliweza kumwabudu Mungu na kumtukuza mbele ya manabii wa Baali, baada ya kukamilisha madhabahu aliyokuwa akiiandaa. Taz (1waf 18:36-39)


         Mungu hushuka na kupokea sadaka ya mioyo yetu, kama kuna maandalizi mazuri ya moyo. Katika agano la kale, sadaka ilitolewa juu ya madhabahu iliyojengwa.


Taz (mwa 22:9) “wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kasha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.”


Kama ilivyoelezewa hapo juu, leo mioyo yetu imefanyika kuwa madhabahu, inayobeba maombi na sifa za Mungu, maana maombi na sifa ni sehemu ya dhabihu au sadaka kati ya nyingi mbele za bwana.
          Kitu kinachochipuka kutoka ndani ya moyo, huwa hakisahauliki na hakipotezi ladha yake. Huwa kina nguvu ya pekee.
           Mara nyingi wanadamu wamekuwa wakiangalia mwonekano wa nje, lakini Mungu hutazama ndani ya mioyo ya watu.

Saturday, July 7, 2012

MAELEZO YA AWALI YA HUDUMA.

Huduma mashuleni ni huduma inayojishughulisha na uinjilishaji wa neno la kristo katika shule mbalimbali za sekondari na vyuo. Huduma hii iko chini ya karesmatiki katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam, hivyo imepewa dhamana ya kuhudumia wanafunzi wanaohitaji huduma za kiroho.

Huduma hii ya uinjilishaji mashuleni, hufanya huduma zake katika siku tofauti katika juma. Wanafunzi hupata nafasi ya kukutana siku ya Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.

Siku ya Jumatatu, wanafunzi au vijana walioamua kujitoa kwa ajili ya Kristo, hukutana kwa ajili ya kujifunza neno la Mungu, lakini siku hii imewekwa maalum kwa ajili ya malezi ya kiroho, hivyo wanafunzi hupata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali ya kiroho.

Siku ya Jumatano, vijana pia hukutana kwa ajili ya kusifu, kuabudu na kusikiliza neno la Mungu. Wanafunzi kutoka shule mbalimbali hufika siku hii kwa ajili ya sala na maombi.

Siku ya Ijumaa pia kunakuwa na kusanyiko la wanafunzi pale Don Bosco Upanga, hukutana kwa ajili ya kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na maigizo na uimbaji. Baada ya darasa hilo kuisha hukutana pamoja kwa ajili ya fellowship ya pamoja.

Siku ya Jumamosi ni siku ambayo wanafunzi wengi hupata nafasi ya kufika kwenye fellowship kwa sababu siku hii wengi huwa hawaendi shuleni. Hivyo hufika Msimbazi Centre kuanzia saa 4:00 asubuhi mpaka saa 8:00 mchana kwa ajili ya maombi pamoja na ushauri. Pia hupata nafasi ya kuonyesha vipawa vyao vya kuimba na kuigiza katika siku hii. Kwa siku ya Jumatatu na Jumatano, hukutana hapohapo msimbazi centre kuanzia saa 10:00 jioni mpaka saa 12:00 jioni.

Pia kila Jumapili ya mwisho wa mwezi huduma mashuleni huandaa siku ya kuishi pamoja ambapo wanafunzi kwa kushirikiana na uongozi wa huduma huiandaa siku hii. Siku hii wanafunzi hufika pamoja na wazazi au walezi kwa ajili ya kusali pamoja, kula pamoja na vijana hao huonyesha mambo mbalimbali wanayojifunza katika huduma ikiwemo michezo inayotumika katika kuinjilisha kama maigizo na nyimbo. Siku hii huitwa siku ya familia, wilaya zote tatu yaani Ilala, Temeke na Kinondoni hukutana pamoja kama familia moja. Pia mbali na kukutana pamoja, familia, yani kila wilaya, hupata nafasi ya kukutana kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ya kimasomo pamoja na kufahamiana zaidi.